RECENT POST
Matokeo ya NEC yateka Dodoma; Wassira atajwa Ukatibu Mkuu
Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Benjamin Mkapa (kushoto) akisikiliza kwa
makini wakati mawaziri mbalimbali walipokuwa wakieleza ufanisi wa wizara
zao kwenye mkutano mkuu wa CCM mjini Dodoma, jana. Pembeni kwake ni
Katibu mkuu wa chama hicho, Wilson Mukama. Picha na Edwin Mjwahuzi
Na Julius Magodi, Habel Chidawali, Dodoma | Mwananchi | Novemba 13 2012
KWA UFUPI
- WASSIRA ATAJWA UKATIBU MKUU,
- WALIOSHINDA WATAMBIANA, WALIOSHINDWA WATOWEKA
WAKATI
matokeo ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), yakiwa yamevuja
baadhi ya wapambe wa wagombea walioshinda wameanza kusherehekea, huku
wengine wakitambiana.
Hata hivyo, matokeo hayo yamekuwa machungu kwa baadhi ya vigogo walioanguka wakiwamo mawaziri, wabunge na watu maarufu.
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuunda sekretarieti
mpya baada ya uchaguzi wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti Bara na
Zanzibar utakaofanyika leo.
Kwa upande wa Zanzibar, matokeo hayo yanaonyesha kuwa walioshinda ni
pamoja na Mbunge wa Uzini, Mohamed Seif Khatib; Waziri wa Afya na Ustawi
wa Jamii, Dk Hussein Ali Mwinyi, Waziri wa Fedha Zanzibar, Omar Yussuf
Mzee, Abdulhakim Chasama na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
(JKT), Shamsi Vuai Nahodha.
Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan,
Khadija Hassan Aboud, Bhaguanji Mansuria, Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa na Khamis Mbeto.
Watu maarufu walioangukia pua katika uchaguzi huo ni Naibu Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Abdallah Juma Sadallah, mtoto wa
Rais Mstaafu, Abdallah Mwinyi ambaye pia ni Mbunge wa Afrika Mashariki,
Mbunge wa Viti Maalumu, Kidawa Salehe na Naibu Waziri wa Fedha wa
zamani, Abdisalaam Issa Khatib.
Walioshinda Bara
Majina ya wajumbe wa Nec walioshinda bara na kura walizopata katika
mabano ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen
Wassira aliyeongoza kundi hilo kwa kupata kura 2,135, Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba (2,093), Mwekahazina
wa CCM, Mwigulu Nchemba (1,967), na Katibu wa UVCCM, Martine Shigela
(1,824).
Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na
Bunge), William Lukuvi (1,805), Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa
Kimataifa, Bernard Membe (1,455), Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na
Uvuvi, Mathayo David Mathayo (1,414), Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Jackson
Msome (1,207), Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama (1,174) pamoja na
Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Fenela Mukangara (984).
Wakati walioshinda Bara na wapambe wao wakitambiana, majina makubwa
yaliyoanguka katika uchaguzi huo ni pamoja ni Mbunge wa Afrika
Mashariki, Shy-Rose Bhanji, Mbunge wa Nkenge, Assumpter Mshama, Richard
Hiza Tambwe na Mbunge wa zamani wa Muleba Kaskazini, Ruth Msafiri.
Wassira atajwa kumrithi Mkama
Habari zilizopatikana jana mjini hapa zinaeleza kuwa Wassira, anatajwa
kuwa anaweza kuikwaa nafasi ya Katibu Mkuu wa chama hicho.
Wengine wanaotajwa kuwa wanaweza kupata nafasi hiyo ya Katibu Mkuu ni
Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye pamoja na Waziri Lukuvi.
Makundi yatambiana
Tambo na kejeli za wapambe, jana zilitawala katika viwanja vya
Ukumbi wa Kizota unakofanyika Mkutano Mkuu wa CCM, baada ya baadhi ya
wajumbe kuanza kusherehekea kutokana na kupata matokeo.
Nje ya ukumbi huo, tangu asubuhi wapambe wa wagombea hao walionekana wakiwa wamekaa katika makundi huku wakinunuliana vinywaji.
Ingawa matokeo yalitarajiwa kutangazwa leo, lakini takriban wajumbe wote
wa mkutano huo walionekana kuyapata hali ambayo iliwafanya walioshinda
kupongezwa wakati wakiingia katika ukumbi wa mikutano.
Mwananchi lilimshuhudia, Waziri Mathayo akipongezwa na baadhi ya wajumbe wa mkutano huo nje ya ukumbi wa mkutano asubuhi.
Pamoja na kupongezwa na wajumbe wa mkutano huo hata washindi wa uchaguzi huo nao walipokutana walipongezana.
Mwananchi lilimshuhudia, Shigela akimpongeza Waziri Wassira na baadaye
walikumbatiana na kupongezana na Nchemba. Baadaye baadhi ya wajumbe
walimbeba Shigela juu juu wakimpa pongezi.
Wakati Shigela akibebwa, baadhi ya wajumbe walimfuata Wassira na
kumpongeza kwa kumshika mikono na wengine kumkumbatia huku yeye wenyewe
akitamba kuwa ni mwarobani wa Chadema.
Waziri Membe akiwa ndani ya ukumbi wa mkutano, baadhi ya wajumbe
wanaomuunga mkono walimfuata na kumzunguka huku wengine wakimkumbatia.
Walioanguka watoweka
Wakati walioshinda wakionekana kufurahi na kupongezwa, hali ilikuwa
tofauti kwa wagombea walioshindwa, kwani baada ya kupata matokeo hayo
wengi walitoweka katika eneo la ukumbi huo.
Kamati ya Uchaguzi yalala ukumbini
Kamati iliyokuwa ikisimamia uchaguzi huo jana ililala katika ukumbi wa
kuhesabia kura kutokana na kazi hiyo kumalizika usiku wa manane, huku
baadhi ya watu waliokuwa wakifanya kazi hiyo kunyang’anywa simu zao ili
matokeo yasivuje.
Watu hao waliondoka katika ukumbi wa kuhesabia kura uliopo katika Ukumbi wa Kizota saa 12:00 asubuhi.
No comments:
Post a Comment
PLEASE COMMET USING APPROPRIATE WORLDS.
THANKS FOR MAKING THIS BLOG YOURS
Note: Only a member of this blog may post a comment.