RECENT POST
HOJA BINAFSI YA KABWE ZUBERI ZITTO(MB) KUHUSU KULITAKA
BUNGE KUCHUNGUZA NA KUILEKEZA SERIKALI KUCHUKUA HATUA DHIDI YA RAIA WA
WATANZANIA WALIOFICHA FEDHA NA MALI HARAMU NJE YA NCHI
[Chini ya Kanuni ya 54(1) na (2)]
UTANGULIZI:
Mheshimiwa Spika,
Mnamo tarehe 2 Novemba 2012 niliwasilisha barua ya kusudio la
kuwasilisha Bungeni Hoja binafsi kuhusu suala hilo hapo juu. Lengo la
Hoja binafsi hiyo ni kuitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, kuwasiliana na Taasisi ya Benki ya Dunia kupitia kitengo cha
‘Assets Recovery’ kurejesha fedha haramu zilizofichwa na Raia wa
Tanzania katika mabenki huko nchini Switzerland. Ofisi yako ilinitaka
nilete maelezo ya ziada kuhusu hoja hiyo ili ipatiwe nafasi ya kupangwa
kwenye ratiba za Bunge. Baada ya kuleta maelezo hayo Ofisi yako imenipa
nafasi kuwasilisha hoja hii mbele ya Bunge lako tukufu. Kwa heshima na
taadhima ninawasilisha mbele ya Bunge lako tukufu hoja hii muhimu sana
katika kuhakikisha kwamba Taifa letu linaziba mianya ya ufisadi na
hususani utoroshwaji wa fedha za kigeni za Tanzania.
Mheshimiwa Spika,
Mwezi Juni mwaka 2012, Benki Kuu ya Switzerland (National Bank of
Switzerland) ilitoa taarifa kwa umma kuhusu raia wa mataifa mbalimbali
duniani wenye dhamana kwenye mabenki nchini humo. Benki hiyo ilitangaza
kwamba Jumla ya dola za Kimarekani milioni 196 (milioni mia moja tisini
na sita) zilikuwa zimehifadhiwa kwenye akaunti za mabenki mbalimbali
nchini humo na kwamba wenye fedha hizo ni Raia wa Tanzania. Fedha hizo
ni zaidi ya shilingi bilioni 314 (mia tatu kumi nanne bilioni)
ukizibadilisha kwa thamani ya fedha za Tanzania.
Mheshimiwa Spika,
Mazungumzo yangu ya mwisho niliyoyafanya jana usiku na wachunguzi waangu
binafsi yameongeza taarifa ya ziada muhimu. Kwanza, kiwango cha fedha
kinacho milikiwa na watanzania nchini Switzerland peke yake ni takribani
mara 20 ya kiwango kilicho tangazwa na Benki ya Tanifa ya nchi hiyo.
Kwa mfano, Benki ya UBS peke yake ina maofisa 240 wanaohusika na
Tanzania peke yake. Kila ofisa mmoja husimamia mteja mwenye kiwango
kisicho pungua dola za marekani milioni 10.
Fedha hizi ni sehemu tu ya fedha ambazo watanzania wanazificha katika
mabenki mbalimbali ya nje ya nchi, na ndani ya hesabu hizi hamna fedha
zilizo nchi nyingine,kama visiwa Jersey, Mauritius na Cayman Islands
maana nchi nyingine hazina utaratibu huu wa kuweka wazi kama ilivyo kwa
nchi ya Swistzerland kwa mwaka huu.
Mheshimiwa Spika,
Gazeti la The Guardian On Sunday la tarehe 23 Juni 2012 lilimnukuu
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ndugu Edward
Hosea akisema kwamba siku ya jumatatu tarehe 24 Juni mwaka 2012
angeandika Barua kwenda Mamlaka za Switzerland kutaka kupewa orodha ya
majina ya raia wa Tanzania wenye fedha katika akaunti zilizotajwa. Hata
hivyo mpaka ninaleta maelezo haya umma wa Watanzania haujalezwa kama
barua hiyo iliandikwa na majibu yake yalikuwa ni nini. TAKUKURU ndio
mamlaka pekee hapa nchini ambayo inaweza kupata orodha ya majina ya watu
wenye mabilioni haya kwa njia za halali na hasa kwa watu ambao ni
‘Politically Exposed Persons’ kama Wabunge na waliowahi kuwa wabunge,
Mawaziri na waliowahi kuwa Mawaziri na viongozi wengine wa ngazi za juu
katika Taifa letu.
Mheshimiwa spika,
Nchi nyingine duniani zimetumia njia mbali mbali kuhakikisha fedha
haramu zinazo toroshwaa zinarejea nchini kwao. Marekani na Ujerumani wao
waliamua kununua CDs kutoka kwa waliokua wafanyakazi wa mabenki ya
Switzerland, wakagundua Raia wao walioficha fedha nje na kuwatoza kodi
kutokana na fedha hizo. Ujerumani wao wameingia mkataba wa kupashana
taarifa za kikodi na nchi ya Switzerland ili kuwatoza kidi raia wao
wenye fedha huko. Hata hivo mkataba huu wa kikodi haujapitishwa na Bunge
la Ujerumani Bundesrat kwani chama kikuu cha upinzani cha SPD
kinapinga, na tayari chama hicho kimenunua CDs zenye majina ya Raia wa
Ujerumani wenye akiba nje.
Hivi karibuni gazeti moja nchini Ugiriki limechapisha orodha ya wagiriki
walioficha fedha zaio huko Switzerland. Orodha hii inatokana na orodha
ambayo alie kua Waziri wa Fedha wa Ufaransa Christine Lagarde aliipa
serikali ya Ugiriki, lakini serikali hiyo haikuifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika,
Kiufupi, toka taarifa za Benki ya Taifa ya Switzerland kutangazwa,
Serikali haijachukua hatua yeyote ya maana kuhakikisha kuwa suala hili
linafanyiwa uchunguzi wa kina na hatua stahili dhidi ya watoroshaji wa
fedha hizo zinachukuliwa ikiwemo kurejeshwa kwa fedha hizo nchini kwa
ajili ya maendeleo ya Taifa letu. Ikumbukwe kwamba katika watanzania
wenye fedha huko nje wapo ambao fedha zao wamezipata kihalali kutokana
na shughuli za kibiashara na wapo ambao wamepata fedha hizi kwa njia za
rushwa. Uchunguzi wa kina ni muhimu sana ili kuweza kutofautisha kati ya
Fedha haramu na fedha halali. Vilevile uchunguzi unatakiwa kutofautisha
katika watu wenye fedha halali kama walifuata taratibu za kisheria za
nchi zinazoruhusu raia wa Tanzania wanaoishi Tanzania kuwa na akiba ya
fedha za kigeni nje ya Tanzania. Kitendo cha Serikali kukaa kimya bila
kuchukua hatua kinaashiria ama kutotimiza wajibu au kwamba wanaopaswa
kuchukua hatua ni washirika wa utoroshaji huu wa fedha za nchi na
kuzificha katika mabenki ya nje.
Mheshimiwa Spika,
Kabla ya kueleza kwa kina vyanzo viwili vikubwa vya fedha kwa raia wa
Tanzania wanaomiliki fedha na mali katika mabenki nje ya nchi nieleze
kwamba, Watu hufungua akaunti nje ya nchi au kumiliki mali nje ya nchi
kwa sababu kuu mbili. Moja ni kuficha fedha haramu zilizopatikana kwa
njia zisizo halali na mbili kukwepa kodi kutokana na mapato yao. Njia ya
kwanza hutumiwa zaidi na wanasiasa na watendaji wa Serikali
(Politically exposed Personalities – PEPs) na njia ya pili hutumiwa na
wafanyabiashara wakubwa na hasa wafanyabiashara wanaouza bidhaa nje ya
nchi. Harakati zozote za kuchukua hatua dhidi ya makundi haya yana faida
ya kuzuia ufisadi kwa kuonyesha kwamba hakuna pa kujificha iwapo
ukifanya ubadhirifu, na kuongeza mapato ya Serikali kwa kuhakikisha Raia
wote wakazi wanalipa kodi inavyostahili.
Uchunguzi wa chanzo cha Fedha.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Taarifa ya Global Financial Integrity (GFI) ya mwaka 2008,
jumla ya dola za kimarekani bilioni 8 (dola bilioni nane) zimetoroshwa
kutoka Tanzania kati ya mwaka 1970 mpaka 2008. Kwa bei ya sasa ya dola
za kimarekani fedha hizi ni sawa na shilingi trilioni 13 (trilioni kumi
na tatu). Mpaka Mwezi Julai mwaka 2012 Deni la Taifa kuanzia mwaka 1961
lilikuwa ni dola za kimarekani bilioni kumi. Hii maana yake ni kwamba
fedha zote zilizotoroshwa kutoka Tanzania katika kipindi cha miaka 38
kingeweza kulipia asilimia themanini ya Deni la Taifa. Mwaka 2012/2013
Bunge limeidhinisha jumla ya shilingi trilioni 1.9 kulipia Deni la
Taifa.Suala hili ni changamoto kwa nchi mbalimbali za kiafrika ambapo
mabilioni yafedha hutoroshwa kila mwaka na watawala wala rushwa na
wafanyabiashara wasio waaminifu kwenda nje ya Afrika na kuliacha bara la
Afrika likiwa na ufukara wa kutupwa.
Mheshimiwa Spika,
Sehemu ya Fedha hizi zilizotoroshwa zilitokana na ufisadi, nyingine
zilitokana na ukwepaji wa kodi na nyingine zilitokana na madeni ambayo
Serikali iliingia ambapo sehemu kubwa ya Madeni ilibaki huko huko
ughaibuni lakini bado Watanzania wanalipa madeni hayo. Hata hivyo Fedha
zilizotokana kutokana Ufisadi na zile za ukwepaji kodi ni nyingi zaidi
katika fedha zilizotoroshwa kutoka Tanzania.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mfano kati ya mwaka 2003 - 2005 Tanzania iligubikwa na ufisadi
mkubwa sana wa Fedha kutoka Benki ya Tanzania ambapo jumla ya shilingi
bilioni 155 zililipwa kutoka Benki Kuu ya Tanzania kwenda Benki ya
NedBank ya Afrika Kusini kama malipo ya mkopo ambao Serikali iliudhamini
kwa ajili ya mradi wa uchimbaji dhahabu wa meremeta. Fedha hizi
zilikuwa ni mara kumi na tano ya mkopo uliodhaminiwa na Serikali.
Uchunguzi wetu unaonesha kuwa asilimia 70 ya fedha za mradi wa meremeta
ziliishia kwenye Benki nchini Switzerland kupitia nchi ya Mauritius.
Mheshimiwa Spika,
Kampuni ya Meremeta ambayo baadaye ilibadilishwa jina na kuitwa TanGold
ilianzishwa kama mradi wa kutorosha mabilioni ya fedha za nchi kwenda
kwa uhusika mkubwa sana wa Serikali. Nawasilisha mezani kwako barua
kutoka Ofisi ya Rais Ikulu ya tarehe 20 Agosti 2001, yenye kumbukumbu
nambari SHC/M.100/4/A kwenda Benki ya Deutsche Bank tawi la Uingereza
kuitambulisha Kampuni ya Meremeta na Kampuni ya Nedcor Trade Services
Limited ya Afrika ya Kusini ili ipewe mkopo. Barua hiyo inatambulisha
miradi miwili ya dhahabu (mgodi wa Tembo na Mgodi wa Buhemba) kwamba ni
miradi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Baada ya barua hii
yaliyotokea ni mtandao mpana wa kuiba fedha za Tanzania kwenda Afrika
Kusini, baadaye Mauritius na kisha kuishia kwenye akaunti za watu
binafsi nchini Switzerland na visiwa vingine vya ukwepaji kodi (tax
havens). Kufuatilia barua hii kutoka Ikulu, mkopo wa dola za kimarekani
milioni kumi zilipatikana. Hata hivyo Serikali ya Tanzania kupitia Benki
Kuu ya Tanzania iliilipa Benki ya NedBank jumla ya dola za Kimarekani
138 milioni, dola milioni kumi kati ya hizi zililipwa kupitia kampuni ya
Deep Green Finance.
Mheshimiwa Spika,
Nilifanya uchunguzi binafsi kuhusu suala hili. Nilijaribu kuwasiliana na
Benki ya NedBank ili kuweza kupata uhakika wa watu waliofaidika na
uchotaji huu mkubwa na wa kihistoria wa fedha za umma. Ufuatiliaji huu
umeendelea vya kutosha ila haujafika mwisho Hata hivyo taarifa
nilizokusanya hadi sasa zimeonyesha hatari kubwa namna ambavyo
watanzania wenzetu wenye mamlaka wanavyokwapua fedha za umma kwa faida
yao. Nyaraka zote za wizi na utoroshaji huu wa fedha na mawasiliano
yangu na watu wa Benki ya NedBank nitayawasilisha mbele ya Kamati ya
Bunge ninayopendekeza kuundwa ili kutazama suala hili.
Mheshimiwa Spika,
Kuna masuala yanayohusu usalama wa nchi kutokana na kashfa hii ambayo
pia ningependa kuyaonyesha katika Kamati ninayopendekeza kuundwa.
Nyaraka hizo zinaonyesha silaha na aina za silaha zilizonunuliwa na
kutoka nchi gani na kwamba silaha hizo ziliishia wapi. Nimeona kwamba
kuyasema masuala haya waziwazi kunaweza kuhatarisha usalama wa nchi
yetu. Hata hivyo masuala haya ni lazima yafahamike ili hatua stahili
ziweze kuchukuliwa dhidi ya watendaji wa Serikali watakaokutwa na
makosa.
Mheshimiwa Spika,
Fedha zilizoibwa na kutoroshwa kupitia kampuni ya Meremeta na kampuni ya
Deep green ziliishia kwenye akaunti za watu binafsi nje ya nchi. Hata
hivyo mara baada ya kuundwa kwa kampuni ya TanGold, jumla ya dola za
kimarekani milioni kumi ziliwekwa kwenye akaunti ya Kampuni hiyo katika
Benki ya NBC, Corporate Branch. Nambari ya akaunti hiyo pia itatolewa
katika kamati ninayoomba kuunda kwa ajili ya uchunguzi wa kina.
Mheshimiwa Spika,
Mwaka 2004, 2006 na 2007 Tanzania iligawa vitalu vya kutafuta mafuta na
Gesi katika maeneo mbalimbali nchini. Uchunguzi wetu unaonyesha kuwa
zaidi ya dola za kimarekani milioni 56 zililipwa kwenye akaunti za watu
binafsi nchini Switzerland kutoka kwenye kampuni zilizoshinda zabuni ya
kutafuta mafuta na gesi.
Mheshimiwa Spika,
Uchunguzi nilioufanya kwa msaada wa wachunguzi waliobobea kwenye masuala
ya mifumo ya kifedha ya Kimataifa umeniwezesha kupata nyaraka muhimu
zinazoonyesha watu na namna walivyopata fedha walizoweka katika akaunti
zao nje ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2004 na 2005 Mwanasiasa wa Afrika Kusini kutoka
chama cha ANC bwana Tokyo Sexwale alitembelea nchini katika ziara ya
kibiashara. Alileta marafiki zake wawili na kuanzisha kampuni iitwayo
Ophir Energy Tanzania limited. Kampuni hii inamiliki vitalu 3 katika
pwani ya bahari ya Hindi blocks 1,3,4. Bwana Tokyo Sexwale
alitambulishwa hapa nchini na raia wa Kongo aitwaye Moto Mabanga. Hivi
sasa bwana Moto Mabanga ameishitaki kampuni ya Ophir Energy kwa
kutotimiza masharti waliyokubaliana kuhusiana na kufanikisha kupatikana
kwa vitalu hivyo vya mafuta. Moto Mabanga ndio alikuwa ‘deal maker’wa
kampuni hii na ili kufanikisha hali hii alihonga sana wanasiasa na
maafisa wa Serikali wanaohusika na ugawaji wa Vitalu vya kutafuta Mafuta
na Gesi. Wakati Ophir wanapewa vitalu hivi sehemu ya hisa za kampuni
hii ziligawiwa kwa baadhi ya watanzania ikionekana kuwa ni hisa kwa
ajili ya chama cha CCM. Hata hivyo uchunguzi wetu unaonyesha kuwa hisa
hizo zilikuwa ni za watu binafsi. Hivi sasa hisa zimeuzwa na fedha
kufichwa katika mabenki mbalimbali nje ya Tanzania. Kuna haja ya kufanya
uchunguzi wa kina kuhusu umiliki wa kampuni ya Ophir Energy wakati
wanaingia nchini na mabadiliko ya umiliki katika kipindi cha miaka
minane iliyopita. Vile vile uchunguzi unapaswa kufanywa kwa vitalu vyote
vilivyogawiwa katika ya mwaka 2003 mpaka 2008 na umiliki wa Watanzania
katika makampuni yaliyopewa vitalu hivyo.
Mheshimiwa Spika, serikali yetu iagizwe na Bunge lako tukufu kupata
taarifa za kina kupitia njia za kiserikali na njia za wachunguzi
binafsi. Mimi kama Mbunge nilipofikia sasa nahitaji msaada wa Bunge
kufanikisha jambo hili. Nilipofikia sasa ni kutoa taarifa na nyakara
zote nilizo nazo na watu TAASISI zitakazo saidia kwa kamati teule ambayo
Bunge litaunda kushughulikia suala hili mahususi.
Baada ya maelezo hayo, naomba kuwasilisha,
HOJA BINAFSI YA KABWE ZUBERI ZITTO (MB) KUHUSU
KULITAKA BUNGE KUCHUNGUZA NA KUILEKEZA SERIKALI KUCHUKUA HATUA DHIDI YA
RAIA WA WATANZANIA WALIOFICHA FEDHA NA MALI HARAMU NJE YA NCHI
[Inatolewa chini ya Kanuni ya 54(3)]
Mheshimiwa Spika,
KWA KUWAkumekuwa na uthibitisho kutoka Mamlaka za nchi ya Switzerland
kwamba kuna raia wa Tanzania wanamiliki fedha za kigeni katika Benki
nchini na kwamba kuna kanuni na taratibu za nchi zinazoendesha na
kuongoza ufunguaji wa akaunti za fedha za kigeni nje ya Tanzania kwa
Watanzania wakazi (residents). Na kwamba kitendo kilichofanywa na
wahusika kuweka mabilioni ya fedha kwenye nchi za nje kinaweza kuwa ni
kinyume na sheria ya “FOREIGN EXCHANGE ACT, 1992”
NA KWA KUWA sheria hiyo kifungu cha (10) cha Sheria ya Fedha za kigeni
kinazuia utoroshaji wa fedha za kitanzania na isipokuwa kwa kibali cha
Gavana wa Benki Kuu tu, hakuna mtu yeyote atakaye ruhusiwa kusafirisha
fedha nje ya Tanzania. Na kinaeleza kuwa kwa msafiri anayekwenda nje ya
nchi hatoruhusiwa kuondoa na kiasi cha shilingi ambazo zinazidi dola za
kimarekani hamsini. Vile vile kwa mujibu wa Sheria hiyo kifungu cha 6 na
7 na waraka uliotolewa na Gavana wa Benki Kuu kwamba Mtanzania yeyote
mwenye kutaka kufungua akaunti kwenye mabenki nje ya Tanzania lazima
apate kibali cha Gavana.
NA KWA KUWA masharti hayo ya sheria yanaweza kuwa yamekiukwa na wahusika kwa kuhifadhi fedha za kigeni katika mabenki ya nje,
NA KWA KUWA ukiukwaji huo ni dhahiri kuwa fedha zilizowekwa kwenye
mabenki ya nje kwa kiasi kikubwa ni fedha ambazo hazikupatika kwa njia
za halali na kwamba kuna uwezekano wa ukwepaji mkubwa wa kodi,
NA KWA KUWA, nchi yetu imekuwa katika matatizo makubwa ya fedha za
kigeni, jambo ambalo limepelekea nchi kushusha thamani ya shilingi ili
kukabiliana na gharama za manunuzi ya bidhaa nje ya nchi,
NA KWA HIYO BASI, ninaliomba Bunge hili liazimie:
1. Kwamba Bunge lako tukufu liunde Kamati Teule kuchunguza Raia wa
Tanzania wenye kumiliki fedha za kigeni na mali nje ya Tanzania. Kamati
Teule hiyo ifanye kazi zifuatazo:
- Kuchunguza mfumo mzima wa utoroshaji wa fedha na kufichwa nje ya nchi,
- kuchunguza na kupembenua mali na fedha haramu dhidi ya halali
zinazomilikiwa na raia wa Tanzania katika taasisi za kifedha nje ya
Tanzania,
- kuchunguza utaratibu mzima wa kugawa vitalu vya utafutaji mafuta na gesi kati ya mwaka 2003 mpaka 2008,
- kuchunguza mtiririko mzima wa utoroshaji wa fedha kutoka Benki Kuu ya
Tanzania kupitia Kampuni ya Meremeta (pia Triannex pty ya Afrika Kusini
na Deep Green Finance ltd) na kupendekeza hatua za kuchukua dhidi ya
wahusika wote wa utoroshaji wa fedha kwenda nje,
- kuchunguza umiliki wa wa watanzania kwenye kampuni zote zenye mikataba
ya utafutaji wa Mafuta na Gesi hapa nchini na namna umiliki huo umekuwa
ukibadilika, mapato (proceeds) zilizotokana na mabadiliko hayo ya
umiliki na kama kodi stahili zimekuwa zikilipwa kutokana na kubadilika
kwa umiliki huo,
- kuchunguza kwa kina mali za Watanzania wote waliowahi kushika nafasi
za Uwaziri Mkuu kati ya mwaka 2003 mpaka 2010, waliowahi kushika nafasi
za Uwaziri wa Nishati na Madini, Uwaziri wa Ulinzi, Ukuu wa Majeshi,
Ukatibu Mkuu wa wizara ya Nishati na Madini, Ukatibu Mkuu wa Wizara ya
Ulinzi, Uanesheria Mkuu wa Serikali, Ukamishna wa Nishati, Ukurugenzi
Mkuu wa TPDC, Uenyekiti na Ujumbe wa Bodi wa TPDC katika ya mwaka 2003
mpaka 2010.
2. Kwamba Serikali ilete muswada wa Sheria Bungeni ifikapo Mkutano wa 11
wa Bunge kwamba itakuwa ni marufuku kwa Kiongozi yeyote wa Umma au mume
au mke wake au watoto wake kuwa na akaunti katika mabenki nje ya nchi
isipokuwa kwa sababu maalumu na kwa kibali rasmi kutoka kwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
3. Kwamba Serikali iwasiliane na Benki ya Dunia ili kupitia Kitengo cha
Assets Recovery Unit mabilioni ya Fedha na mali zisizoondosheka
zinazomilikiwa na Watanzania katika mabenki ya nchini Switzerland,
Dubai, Mauritius na visiwa na maeneo mengine yote ambapo hufichwa fedha
na Mali ili kukwepa kodi na kwamba mali hizo na mabilioni hayo
yaliyopatikana kiharamu yarudishwe nchini mara moja
4. Kwamba katika muswada tajwa hapo juu, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania
aimarishiwe mamlaka ya kutoa kibali kwa Mtanzania yeyote anayetaka
kufungua akaunti ya Benki nje ya nchi na kwamba kila mwaka Gavana
atatangaza kwenye Gazeti la Serikali na magazeti yanayosomwa na wananchi
wengi orodha ya Watanzania walioomba na walioruhusiwa kuwa na akaunti
ya Benki nje ya Tanzania.
5. Kwamba Watanzania wote wenye akaunti za fedha nje waeleze
wamezipataje na TAKUKURU wachukue hatua za kisheria dhidi ya watu wote
wenye kumiliki fedha na mali kinyume na mapato yao halali.
6. Kwamba Serikali, katika mkutano wa Bunge wa 11 na baada ya Taarifa ya
Kamati Teule ya Bunge kuhusu Raia wa Tanzania wenye kumiliki fedha za
kigeni kwneye mabenki na mali nje ya Tanzania ilete taarifa ya hatua
ilizochukua ili kuziba mianya ya utoroshaji wa fedha nje ya Tanzania.
7. Kwamba Serikali katika Bajeti ya mwaka 2013/14 itaanzisha kodi
maalumu ‘financial transaction tax’ ya angalau asilimia 0.5 ya thamani
ya ‘transaction’ ili kuweza kuwa na rekodi za uhakika za fedha ndani na
zinazotoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika,
Naomba kutoa hoja,
…………………….
KABWE ZUBERI ZITTO(MB)
JIMBO LA UCHAGUZI-KIGOMA KASKAZINI
No comments:
Post a Comment
PLEASE COMMET USING APPROPRIATE WORLDS.
THANKS FOR MAKING THIS BLOG YOURS
Note: Only a member of this blog may post a comment.